Je, Kuweka Akiba ni Kukosa Imani?

Watu wengi wanapofikiria kuhusu akiba, huiona kama jambo la kifedha tu. Wengine huihusisha na hofu ya kesho, na wengine huiahirisha wakiamini wataanza “wakipata zaidi.” Katika ulimwengu wa leo wenye changamoto za kiuchumi, wengi wanajiuliza: Je, kuweka akiba ni kukosa imani au ni busara? Hadithi ya Yusufu (Joseph) katika kitabu cha Mwanzo inatoa mwanga wa kipekee kuhusu suala hili. Tunachojifunza kutoka kwa nabii huyu wa Mungu si tu historia bali ni kanuni za milele zinazoweza kubadilisha mtazamo wetu kuhusu akiba na utajiri.
1. AKIBA SI KUKOSA IMANI NI KUTII HEKIMA YA MUNGU.
Watu wengi wanafikiri kuwa kuweka akiba ni ishara ya kuwa na imani ndogo kwa Mungu. Lakini Yusufu anatufundisha tofauti kabisa. Mwanzo 41:33-36 inatuonyesha kwamba imani haibatilishi wajibu; bali imani inampa mtu wajibu na mwelekeo.
Yusufu alipomfasiria Farao ndoto zake, hakusema tu, “Mungu atatunza.” Badala yake, alitoa mpango thabiti wa kiutendaji: kuteua maafisa, kukusanya tano ya mavuno, na kuhifadhi chakula. Imani yake ilimfanya atende kwa busara, si kukaa tu na kusubiri miujiza.
Kanuni: Imani ya kweli hukupa uhodari wa kupanga kwa akili. Usiogope kuweka akiba, ni tendo la utii kwa uongozi ya Mungu.
2. MISIMU MIZURI NI BARAKA, LAKINI PIA NI MTIHANI
Farao aliota ng’ombe saba wanono na masuke saba mazuri, kisha wakaja ng’ombe waliokonda na masuke kame. Ujumbe ulikuwa wazi: “Tazama, miaka saba mikubwa ya neema inakuja... na baada yake miaka saba ya njaa” (Mwanzo 41:29-30).
Tunapofurahia mafanikio na uwepo wa neema, ni rahisi kusahau kwamba hali hiyo si ya kudumu. Miaka mizuri ni mtihani je, utatumia kwa ubadhirifu au kujiandaa kwa wakati mgumu? Yusufu alitumia miaka ya wingi kujiandaa kwa miaka ya uhaba.
Kanuni: Usichukulie mafanikio ya leo kuwa ya milele. Tumia wakati wa “mazuri/neema” kujiandaa kwa “mabaya/dhiki” inayoweza kuja.
3. NIA NZURI HAIKOI PESA, MIFUMO MIZURI NDIO HUOKOA
Watu wengi wana nia njema ya kuweka akiba, lakini nia pekee haihifadhi pesa. Mwanzo 41:34 inasema: “Farao afanye hivi, awaweke maafisa juu ya nchi, na awatoe fungu la tano la mazao ya nchi ya Misri katika miaka saba ya wingi.”
Yusufu hakuwa na nia tu bali aliunda mfumo. Aliteua watu, alianzisha utaratibu wa kukusanya kwa asilimia maalum, na akafungua maghala. Bila mfumo, nia hufa.
Kanuni: Unda mfumo wa kiotomatiki wa kuweka akiba. Weka punguzo la kawaida la mapato yako (kwa mfano, 10%, 20%) kabla ya kutumia chochote. Nia ni nzuri, lakini mifumo ndiyo inayotoa matokeo.
4. WEKA AKIBA KWANZA, SI MWISHO: JAPOKUWA NI BORA KUWEKA HATA MWISHO KULIKO KUTOWEKA KABISA
Yusufu alianza kukusanya tano ya mavuno mwanzoni mwa miaka ya wingi, si baadaye. Hii ndio kanuni ya “kuweka akiba kwanza” (pay yourself first). Watu wengi hungoja hadi mwisho wa mwezi, wanaposalia na chochote, na mara nyingi hakuna kinachosalia.
Lakini pia, Yusufu alianza kukusanya mwaka wa kwanza wa wingi. Hata kama umechelewa kuanza kuweka akiba, bora kuchelewa kuliko kutokuwepo kabisa. Kuanza leo, hata kwa kiasi kidogo, ni bora kuliko kusubiri kesho isiyo na hakika.
Kanuni: Weka akiba kabla ya matumizi. Tenga kiasi ulichokiamua mara unapopokea mshahara wako au unapopata fedha kutoka kwenye vyanzo vyako. Na kama hujaanza, anza leo bado ni wakati mzuri.
5. NIDHAMU YA LEO INAZUIA MAUMIVU YA KESHO
“Njaa hiyo ikawa katika nchi zote... lakini katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula” (Mwanzo 41:54).
Wakati miaka ya njaa ilipofika, watu wa Misri na mataifa ya jirani walikuja kwa Yusufu kununua nafaka. Je, unafikiri walijuta kwa kukosa nidhamu ya kuweka akiba? Watu wengi waliozoea kutumia kila kitu wanapopata, wakati dharura inapotokea wanaumia zaidi. Nidhamu ya leo inauma na kukatisha tamaa, lakini hisia ya kuwa “masikini” wakati wa shida ni chungu zaidi.
Kanuni: Chagua maumivu ya nidhamu sasa badala ya maumivu ya kujuta baadaye. Kuweka akiba kunaweza kukufanya ukahisi kama unajitesa, lakini kuishi mwezi mzima bila senti ni kigumu zaidi.
6. AKIBA INALETA UHURU, SIO KIFUNGO
Watu wengi hudhani kuwa kuweka akiba ni kujifungia maisha. Lakini kwa kweli, akiba huleta uhuru. Inakupa nafasi ya kufanya maamuzi bila kusukumwa na hofu ya dharura. Mwanzo 41:40-41 inaonyesha kuwa usimamizi mzuri wa rasilimali ulileta uthabiti, mamlaka, na usalama. Mtu mwenye akiba anaishi kwa utulivu zaidi kuliko anayeishi kila siku kwa presha ya ukosefu.
Tunaogopa kuweka akiba kwa sababu tunafikiri itatunyima uhuru. Lakini angalia Yusufu: “Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri... Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, mtu hatainua mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri”
Akiba haikumfungia Yusufu, ilimfanya awe na uhuru wa kusaidia familia yake, watawala, na mataifa yote. Akiba inakupa uhuru wa kuchagua, wa kusaidia, wa kulala usiku bila wasiwasi, na wa kusubiri fursa bila kukimbilia maamuzi mabaya.
Kanuni: Tazama akiba kama ufunguo wa uhuru, si kizuizi. Kila shilingi unayoweka akiba ni hatua kuelekea uhuru wako wa kifedha.
7. MAANDALIZI YA DHARURA NI HEKIMA YA KIBIBLIA
Yusufu hakusubiri njaa ije ndipo aanze kupanga. Alijiandaa mapema. “Chakula hicho kitakuwa akiba kwa nchi kwa ajili ya miaka saba ya njaa” (Mwanzo 41:36).
Katika Biblia, kuwa tayari kwa wakati mgumu si kukosa imani bali ni hekima. Tunahitaji hazina ya dharura, bima, na mpango wa siku za mvua. Huwezi kutabiri ajali, ugonjwa, au kupunguzwa kazi, lakini unaweza kujiandaa.
Kanuni: Jenga hazina ya dharura ya angalau miezi 3-6 ya matumizi yako. Hii si hofu ila ni hekima inayotokana na Mungu.
8. AKIBA NI USIMAMIZI, SI UBAHIRI
Watu wengine wanakosoa kuweka akiba kwa kusema ni ubahiri. Lakini Yusufu hakuhifadhi chakula kwa ubinafsi. “Nchi zote zilimjia Yusufu Misri kununua nafaka, kwa kuwa njaa ilikuwa kali katika nchi zote” (Mwanzo 41:56).
Yusufu alitumia akiba kusaidia wengine; familia yake, wamisri, na mataifa ya jirani. Akiba halisi haina ubinafsi; ni zana ya kuwajibika kwa wale tunaowapenda. Kukusanya pesa bila kusaidia ni ubahiri. Lakini kuweka akiba kwa lengo la kusaidia wakati wa dharura, huo ni usimamizi mwema.
Ni muhimu kutofautisha kati ya akiba na uroho. Yusufu hakuhifadhi chakula kwa tamaa, bali kwa wokovu wa watu. Mwanzo 41:56 inaonyesha kwamba kile kilichokusanywa kiligeuka kuwa msaada kwa wengi wakati wa shida. Hivyo, akiba ya kweli si kuficha kwa ubinafsi, bali kusimamia kwa uaminifu kile Mungu amekupa ili kiwe baraka kwako na kwa wengine.
Kanuni: Uliza: Kwa nini ninaweka akiba? Kwa ajili ya familia yangu? Kwa ajili ya kutoa wakati wa shida? Akiba yako iwe na kusudi la huduma.
9. HEKIMA YA FEDHA INAONESHA UKOMAVU WA KIROHO
Farao alipomtazama Yusufu, alisema: “Je, twaweza kumpata mtu kama huyu, ambaye roho ya Mungu imo ndani yake?” (Mwanzo 41:38).
Siri ya Yusufu haikuwa akili za kibiashara tu bali uwepo wa Roho wa Mungu. Jinsi unavyoshughulikia pesa inaonyesha kukomaa kwako kiroho. Mungu anaamini kuweka rasilimali mikononi mwa wale wanaojua kuzitumia kwa ajili ya wengine na kwa utukufu wake.
Mara nyingi tunapozungumzia maisha ya kiroho, tunawaza maombi, ibada, na huduma. Lakini simulizi la Yusufu linatuonyesha kwamba ukomavu wa kiroho huonekana pia kwenye namna mtu anavyosimamia rasilimali. Mwanzo 41:38 inaonyesha kuwa roho ya hekima ndani ya Yusufu ilijidhihirisha katika uongozi na usimamizi wake. Fedha nazo ni kipimo cha uaminifu, nidhamu, na ukomavu.
Kanuni: Mafanikio ya kifedha sio lengo la kiroho, lakini ni kielelezo cha ukomavu wako wa kiroho. Simamia pesa zako kama mtu aliye na Roho wa Mungu.
10. NIDHAMU NDOGO LEO, MATOKEO MAKUBWA KESHO
Watu wengi hudharau hatua ndogo. Wanasubiri siku watakapokuwa na pesa nyingi ndipo waanze kuweka akiba. Lakini maisha hubadilishwa na nidhamu ndogo zinazofanywa kwa uaminifu kila siku. Hata kile kidogo unachotenga leo kinaweza kuwa msaada mkubwa kesho. Wazo la Mwanzo 50:20 linatukumbusha kwamba Mungu anaweza kutumia maandalizi madogo ya leo kuleta manufaa makubwa baadaye. Tunakumbuka maneno ya Yusufu kwa ndugu zake: “Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema” (Mwanzo 50:20).
Kila hatua ndogo ya nidhamu, kukusanya tano ya mavuno mwaka baada ya mwaka, ilijenga msingi wa ukombozi wa taima zima. Nidhamu ndogo za kila siku, kama kuweka akiba asilimia kumi ya mshahara wako kwa mwezi au kipato chako, baada ya miaka inakuwa mlima wa neema.
Kanuni: Usidharau nguvu ya nidhamu ndogo inayorudiwa kwa wakati. Kila beseni unalojaza chakula nyumbani kwako, kila senti unayoweka kwenye akiba sio ndogo mbele ya Mungu.
HITIMISHO:
Yusufu aliishi maisha ya kupanda na kushuka, alikuwa mtumwa, mfungwa, na hatimaye mtawala. Lakini alichojifunza ni kwamba akiba si ishara ya kukosa imani. Akiba ni alama ya imani inayofanya kazi. Leo, unaweza kuanza. Chukua kanuni moja kati ya hizi na uitumie kwa vitendo. Kumbuka: Akiba ya leo ni uhuru wa kesho. Nidhamu ya sasa ni furaha ya baadaye. Na kusudi lako kubwa linapaswa kuwa, kuwabariki wengine kwa yale uliyoyaweka akiba.
Yusufu anatufundisha kwamba kuweka akiba si suala la fedha pekee, bali ni suala la maono, tabia, na uaminifu. Ni kuelewa kwamba Mungu anaweza kukubariki leo, lakini pia anakutazamia usimamie vizuri baraka hiyo kwa ajili ya kesho. Akiba si ishara ya hofu. Akiba ni hekima. Akiba ni utiifu. Akiba ni maandalizi.
“Mwenye kuweka akiba wakati wa wingi, ni mwenye hekima.”
Je, utakuwa mwenye hekima leo?